Chama cha Wapalestina cha Hamas kinachotawala Ukanda wa Gaza kimetangaza uamuzi wa upande mmoja wa kusitisha mapigano, baada ya ghasia baina yake na Israel ambazo ni kubwa zaidi kwa miezi mingi. Inaarifiwa kuwa Misri ilisaidia kufikia uamuzi huo. Tangazo la makundi kadhaa ya wapalestina, Hamas ikiwemo limesema makundi hayo yatasitisha uhasama ikiwa Israel pia itaacha mashambulizi. Ghasia hizi zilianza Jumapili iliyopita kufuatia operesheni ya Israel ndani ya Ukanda wa Gaza ambamo mmoja wa makamanda wa Hamas aliuawa. Hamas ilianzisha mashambulizi ya kulipa kisasi, yaliyosababisha makabiliano yaliyouwa wapiganaji saba wa Hamas na mwanajeshi mmoja wa Israel. Israel ilishambulia Ukanda wa Gaza Jumatatu kwa kutumia ndege za kivita wakati Hamas ikivurumusha mamia ya maroketi Kusini mwa Israel. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana katika kikao cha faragha kujadili kusambaa kwa mapigano hayo lakini hakukua na maafikiano ya namna ya kuukabili.