Shirika la Msalaba Mwekundu linakadiria kuwa watu 400,000 wamepoteza makaazi yao nchini Msumbiji kutokana na Kimbunga Idai kilichoipiga nchi hiyo siku tano zilizopita.
Shirika hilo limesema kiasi kidogo tu cha msaada kinaweza kuwafikia maelfu wanaouhitaji, kwa sababu mvua kubwa zinaendelea kunyesha, zikizidisha athari za mafuriko ambazo tayari ni kubwa.
Barabara, madaraja na mashamba vimesombwa na kimbunga hicho katika nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema yamkini watu 1,000 wameuawa na kimbunga hicho, na ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Shirika la Chakula Ulimwenguni, WFP limesema kimbunga Idai kimepita katika eneo linalokaliwa na Wamsumbiji wapatao milioni 1.7. Watu 920,000 katika nchi jirani ya Malawi wameathiriwa pia na kimbunga hicho, pamoja na maelfu wengine nchini Zimbabwe.