Mizinga na risasi zimefyetuliwa dhidi ya jengo moja kubwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi. Polisi na mashahidi wanazungumzia kuhusu shambulio la kigaidi. Ndani ya jengo hilo kuna Hoteli kubwa inayojulikana kama Dusit D2, benki na ofisi. Magari kadhaa yameshika moto. Watu wanakimbia na wengine kuhamishwa toka eneo hilo. Risasi ziliendelea kufyetuliwa kwa dakika kadhaa, moshi umetanda katika eneo hilo. Msemaji wa polisi Charles Owino amesema maafisa zaidi wa polisi ikiwa ni pamoja na vikosi vya kupambana na ugaidi wamepelekwa katika eneo hilo. Magari ya kusafirisha wagonjwa, na askari wa zima moto wameshapelekwa katika eneo hilo. Wanamgambo wa itikadi kali wa al Shabab wanadai kuhusika na shambulio hilo. Shambulio hilo linakumbusha lile lililotokea mwaka 2013 dhidi ya jengo la maduka ya fakhari la Westgate Mall ambapo wanamgambo hao hao wa itikadi kali wa al Shabab waliwauwa watu wasiopungua 67.