KENYA imejiunga rasmi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mwanachama asiye wa kudumu kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kuanzia Januari Mosi mwaka huu.
Nafasi hiyo pia inaangaziwa kuwa ni muhimu kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Wachambuzi wa masuala ya siasa za Pembe ya Afrika wanasema Kenya ipo katika nafasi nzuri ya kusaidia kutatua migogoro iliyopo katika kanda hiyo.
Miongoni mwa malengo ya Kenya ni kuhakikisha kundi la kigaidi la Al Shabab linaorodheshwa katika kundi la magaidi na Umoja wa Mataifa kama ilivyo kwa kundi la Al Qaeda.
“Kidiplomasia, Kenya inatarajiwa kutumia kiti hicho kuhakikisha inashinda mzozo wake wa kidiplomasia na Somalia kuhusu mpaka wa Bahari ya Hindi,” alisema Musa Odhiambo ambaye ni mchambuzi wa siasa Kanda ya Pembe ya Afrika.
Kuhusu mzozo wa Jimbo la Tigray, alisema Ethiopia itataka kuitumia Kenya kusukuma mzozo huo kuwa ajenda ya kimataifa wakati huu mataifa ya Ulaya yakitaka wasuluhishi wa kimataifa kuingilia kati.
Kenya itashika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambacho kitamalizika mwishoni mwa mwaka 2022. Ilifanikiwa kupata nafasi hiyo baada ya kuishinda Djibouti.
