KRC Genk imetwaa ubingwa wa Ubelgiji kwa mara ya nne.
KRC Genk imetwaa ubingwa wa Ubelgiji kwa mara ya nne, ikiwa ni miaka 20 tangu walipotwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza (1999), na miaka 8 tangu walipoutwaa kwa mara ya mwisho (2011). K.R.C Genk timu anayochezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta imetwaa taji la ligi ya soka ya Ubelgiji baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Anderlecht na kufikisha pointi 51 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine.
Ubingwa huo umepatikana baada ya mahasimu wao Club Brugge kupoteza mchezo wao kwa kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Standard Liege hivyo kupoteza uwezo wa kufikisha pointi 51 huku ukiwa umebaki mchezo mmoja katika mchuano wa timu sita bora.
Samatta ambaye anaongoza kwa ufungaji mabao kwenye ligi hiyo alianza mchezo huo kabla ya kupumzishwa kwenye kipindi cha pili.
Kwa ubingwa huo Genk wamepata nafasi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.