Mbarawa apewa siku saba.

In Kitaifa

RAIS John Magufuli amesema ameanza ziara yake mkoani Rukwa vibaya na kwa majonzi kutokana na ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya Sh bilioni 20 kutelekezwa na mkandarasi Fally Enterprises asiye na sifa wala uwezo ambaye ameagiza achunguzwe na kushitakiwa.

Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuwachukulia hatua kali watendaji wa wizara yake waliohusika kumpatia kazi nyingi zaidi mkandarasi huyo kinyume cha utaratibu.
Aidha, amemwagiza Profesa Mbarawa na kumpatia siku saba kuunda tume maalumu ya wataalamu kuifanyia uchunguzi wa kina miradi yote inayotekelezwa na mkandarasi huyo aikiwamo ile ambayo haijaikamilisha.

Mbali ya Wizara ya Maji, pia ameagiza Tamisemi, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa,Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa na Wakili wa Serikali kufuatilia tuhuma dhidi ya mkandarasi huyo pamoja na hujuma uliyofanywa katika Mradi wa Maji Laela.

Pia amempigia simu na kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Simon Siro kumwondoa Ofisa Mnadhimu, Polycarp Urio kwa kushindwa kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiwa ziarani Rukwa hivi karibuni.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana katika Mji Mdogo wa Laela Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kabla ya kuzindua barabara ya Tunduma – Laela – Sumbawanga ya kilometa 223.2 iliyogharimu Sh bilioni 375.
Mradi huo wa barabara ulikamilika kujengwa tangu mwaka 2015 kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Millennium Challenge (MCC) na fedha za ndani za Serikali ya Tanzania kwa kiwango cha lami.
“Huyu mkandarasi Fally hamalizi ujenzi wa miradi huku mingine ikiwa chini ya kiwango. Nashangaa amepewa miradi yote… lakini
hajafutiwa usajili kwa mujibu wa sheria namba 15 ya 1994,” alieleza Rais Magufuli.

“Waziri andaa tume maalumu ichunguze miradi yote ya maji anayoijenga pia ifanyiwe upya thathmini pamoja na kubaini kama utaratibu
wa manunuzi umefuatwa kwa mujibu wa sheria. Kama mkandarasi huyo amelipwa waziri baada ya kuwasilisha certificate zote mlipaji
awekwe ndani kwa mujibu wa sheria,” alizidi kuagiza Rais Magufuli.

Alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kumfuatilia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli kama amemlipa mkandarasi huyo.
Mkandarasi huyo anatuhumiwa kuhujumu miradi ya maji kwa kuijenga kwa viwango hafifu ukiwemo mradi wa maji wa Laela wa gharama.

ya zaidi ya Sh bilioni 1.7 ukiwa umemalizika miaka mitatu iliyopita lakini maji hayatoki.
Miradi hiyo iko katika wilaya za Kalambo, Nkasi na Sumbawanga.

“Ninazo taarifa kuwa Waziri Profesa Mbarawa ulipokuwa mkoani Rukwa kikazi uliagiza mkandarasi Fally akamatwe lakini akaachiwa. Nataka nimfahamu nani aliyemwachia huru akikaidi agizo la waziri ambaye ni mteule wangu,” amehoji huku akiwataka viongozi
wasitishwe na watu wenye fedha.

Awali, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy alimweleza Rais Magufuli kuwa mkandarasi Fally hana sifa wala viwango, na amefisadi miradi ya maji huku akijilimbikizia mali kwa kujenda maghorofa sehemu mbalimbali.
“Mheshimiwa Rais mafisadi kama Fally wanastahiki adhabu kali ya kunyongwa… Pia azitapike fedha zote kama wengine wanavyozitapika,” alisema mbunge huyo machachari.

Baada ya kuzindua barabara, Rais alifika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Laela na kumpigia IGP Sirro na kumuagiza amfukuze
Mnadhimu Urio kwa kushindwa kumpatia RPC majina tisa ya askari polisi ambao Waziri Lugola aliagiza wahamishwe kwa makosa ya kuwabambikizia kesi wananchi na kuwanyima dhamana.
Rais Magufuli ambaye alitokea mkoani Songwe alikokuwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, jana alianza ziara mkoani Rukwa ambayo inaendelea leo. Akimaliza mkoa huo atakwenda kwa ziara nyingine Mkoa wa Katavi.

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu