Wabunge katika bunge la Umoja wa Ulaya wametoa wito kwa serikali ya Uingereza kufikiria vizazi vijavyo na kusalia katika Umoja huo. Katika barua ya wazi iliyonukuliwa na shirika la habari la Funke nchini Ujerumani, zaidi ya wabunge 100 wa Umoja huo wameitaka Uingereza iuache mchakato wa kuiondoa nchi yao maarufu kama Brexit. Wabunge hao wamesema uamuzi kama huo utapokelewa vyema katika Umoja wa Ulaya. Rasimu ya barua hiyo inatarajiwa kuchapishwa Uingereza leo kabla kura muhimu itakayopigwa katika bunge la Uingereza kuhusu rasimu ya mpango wa Brexit ya Waziri Mkuu Theresa May. Waangalizi wanasema May hana uungwaji mkono wa kutosha kwa rasimu hiyo kupita. Baadhi ya wabunge wa Uingereza wamependekeza kusogezwa mbele kwa siku ya mwisho ya Brexit ambayo ilikuwa imepangiwa kuwa Machi 29. Lakini mgombea mkuu wa chama cha European People’s Party, Manfred Weber amesema nyongeza hiyo ya muda haistahili kuvuka tarehe ya uchaguzi wa bunge la Ulaya mwezi Mei.