Serikali ya Msumbiji imesema hali katika maeneo yaliyokumbwa na kimbunga Idai imeanza kuwa nzuri kuruhusu msaada wa dharura kupelekwa haraka kwa watu wanaouhitaji. Imesema barabara muhimu inayoelekea katika mji wa Beira hivi sasa imefunguliwa, na msaada wa kimataiafa unaanza kumiminika. Jeshi la Marekani limesema litaungana na mashirika ya kimataifa ya wahisani katika kusambaza madawa na chakula kwa waathiriwa wa kimbunga hicho kilichosababisha maafa makubwa ya kiasili kuwahi kuukumba ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa miongo mingi. Waziri wa mazingira wa Msumbiji Celso Correia amesema watu 228,000 wamewekwa katika kambi katika eneo kubwa la Msumbiji lililofurika. Kumeripotiwa mripuko wa magonjwa ya kuhara, lakini waziri Correia amesema bado ni mapema kujua ikiwa ugonjwa huo ni kipindupindu. Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na kimbunga Idai imefika watu 761, kati ya hao 446 wakiwa kutoka Msumbiji, 259 kutoka Zimbabwe, na 56 wakiwa Wamalawi.