Mwandishi habari wa Urusi aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa kile alichokiita kuwa ni vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na Urusi nchini Georgia, Crimea, Mashariki mwa Ukraine na Syria, alipigwa risasi jana mgongoni nyumbani kwake mjini Kiev. Arkady Babchenko alifariki dunia wakati akipelekwa hospitali. Polisi ya Ukraine imesema mke wake alimkuta akiwa chumbani akivuja damu. Babchenko aliyekuwa na umri wa miaka 41, aliondoka Urusi mwaka wa 2017, akikabiliwa na miito ya kupokonywa uraia wake na kuongezeka kwa vitisho dhidi yake kutokana na maoni yake kuhusu ajali ya ndege ya Desemba 2016 ambayo iliwauwa waimbaji wa kwaya ya heshi la Urusi waliokuwa njiani kwenda Syria kuwatumbuiza marubani wa jeshi. Alituhumiwa kwa kukosa uzalendo, kitu alichosema kuwa kinashangaza ikizingatiwa kuwa aliipigania nchi yake katika vita vya kwanza ya kutaka kujitenga nchini Chechnya katika miaka ya 1990. Wanasiasa wanaoiunga mkono serikali walianza kumkana na kutaka afungwe jela kutokana na maoni yake.