Chombo cha anga za mbali cha Marekani kisicho na abiria kimetua jana kwenye sayari nyekundu ya Mirihi au Mars baada ya safari ya kiasi kilometa milioni 480 kikilenga kukusanya data juu ya iwapo kulikuwa viumbe hai miaka iliyopita. Shirika la taifa la Marekani linaloshughulikia utafiti wa anga za mbali NASA imethibitisha kutua kwa chombo hicho jana usiku baada ya karibu miezi saba ya safari ngumu kuifikia sayari ya Mirihi.
Kuanzia msimu wa kiangazi chombo hicho kinachotumia teknolojia mamboleo, kitajaribu kukusanya mawe na mchanga utakaorejeshwa duniani kabla ya mwaka 2030 kwa ajili ya utafiti zaidi wa kisayansi. Kutua kwa chombo hicho cha Marekani ni tukio la tatu la kutumwa chombo cha anga za mbali kwenye sayari ya Mars katika muda wa zaidi ya wiki moja. Siku kadhaa zilizopita vyombo viwili vya anga za mbali vinavyomilikiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu na China viliwasili kwenye mzingo wa sayari hiyo kwa ajili ya utafiti.
