Raia wa Nigeria wanaoishi Afrika Kusini wamepewa ofa ya usafiri wa ndege wa bure kabisa kurejea nyumbani kujinusuru na vurugu za kibaguzi zinazoendelea Afrika Kusini.
Wizara ya mambo ya Nje ya Nigeri imesema mmliliki wa Shirika la Ndege la Air Peace yupo tayari kuwasafirisha bure wale wote watakaotaka siku ya Ijumaa.
“Wote watakaotaka huduma hiyo wanashauriwa kuwasiliana na Ubalozi wa Nigeria jijini Pretoria na ofisi ndogo za ubalozi jijini Johannesburg kwa matayarisho muhimu,” taarifa ya wizara imeeleza.
Mashambulizi ya biashara zinazomilikiwa na wageni nchini Afrika Kusini zimepokelewa kwa hasira kali na Wanaigeria ambao wanahisi wanalengwa na kuonewa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Geoffrey Onyeama amewaambia wanahabari siku ya Jumatano kuwa kulingana na taarifa zilizowafikia, hakuna raia wa Nigeria aliyepoteza uhai kwenye ghasia zinazoendelea.
Hata hivyo, amesema kuwa serikali inaangalia uwezekao wa kumrejesha nyumbani balozi wake kutoka Afrika Kusini na kudai fidia kwa biashara zote za raia wa nchi hiyo zilizoshambuliwa.