Nyusi ametua wilayani Chato, Mkoani Geita Kaskazini mwa Tanzania na kupokewa na mwenyeji wake rais Dkt.John Magufuli.
Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Prof Palamagamba Kabudi ameielezea ziara hiyo kuwa ya kindugu ambayo itaangazia masuala ya kidiplomasia na biashara. Waziri huyo ameeleza kuwa ziara hiyo ilipangwa kufanyika mwaka jana lakini ikashindikana kutokana na uchaguzi wa Tanzania.
Japo Waziri Kabudi hakutanabahisha mbele ya wanahabari jana Jumapili iwapo suala la usalama katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji litakuwa sehemu ya majadiliano, bila shaka viongozi hao watajadili suala hilo.
Serikali ya Tanzania mwaka jana ilituma vikosi vyake vya jeshi ili kujihami na tishio hilo la ugaidi.
Wanamgambo wa Kiisilamu wenye mafungamano na kundi la IS wanaendesha shughuli za kigaidi kaskazini mwa Msumbiji kwenye jimbo la Cabo Delgado na mara kadhaa wamevuka mpaka na kushambulia vijiji vya Tanzania.
Mwezi Oktoba mwaka jana magaidi hao walifanya shambulio katika Kijiji cha mpakani cha Kitaya mkoani Mtwara. Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa Tanzania IGP Simon Sirro magaidi zaidi ya 300 walivuka mpaka na kufanya uhalifu ikiwemo mauaji.
Sirro alithibitisha kuwa baadhi ya washukiwa wa ugaidi waliokamatwa walikuwa ni raia wa Tanzania.
