TAMKO KWA WANAHABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2020

In Kitaifa


Dar es Salaam Agost 12, 2020. Wakati macho na masikio ya Watanzania yakiisubiri kwa hamu Oktoba 28 ambayo ni siku ya uchaguzi mkuu nchini, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) tunaoa mapendekezo kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa.
Uchaguzi Mkuu unafanyika wakati ambapo kati ya wagombea 16 waliochukua fomu kugombea urais, wapo wanawake wawili mpaka sasa ambao ni Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC, na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini walioteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo. Kadhalika, wapo wanawake watano wanaowania umakamu wa Rais, katika mchakato huu wa uchaguzi.
Lakini TAMWA, WiLDAF na GPF taasisi ambazo malengo yake ni kuwepo kwa jamii yenye amani, inayoheshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia, na amani zimeona ni vyema kuikumbusha jamii, wadau wa masuala ya siasa na ya jinsia kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ushiriki duni wa wanawake katika siasa.
TAMWA WiLDAF na GPF chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’ imeendesha midahalo mbalimbali ya wanawake kutoka vyama vya siasa ,wakiwamo wanawake wanasiasa, viongozi wa dini na kubaini kuwa bado kuna changamoto zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa.
Midahalo tuliyofanya katika kanda za Dodoma, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam, iliibua changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ikiwamo lugha dhalilishi zinazowavunja moyo wanawake wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.
Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni, na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma. Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake, Rose Reuben, Mkurugenzi TAMWA.
Katika midahalo hiyo, TAMWA , WiLDAF na GPF tumebaini kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbali mbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Hii ni pamoja na tabia za wajumbe wanaotegemewa kupiga kura kuwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa kitu kidogo ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea. Hii inaathiri wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana.

Pia tumebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.Changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.
Hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo na hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.
Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono na pia tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu.
Pia tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake.
Changamoto nyingine zilizoibuliwa katika midahalo hiyo, ni Ilani za vyama vya siasa ambazo hazitoi nafasi kwa wanawake kuwa viongozi na kupata nafasi ya kugombea katika majimbo. Tumebaini wanawake wengi wanashindwa kushiriki uchaguzi kwa kutopata baraka hii kuanzia ndani ya vyama.
Wakati huo huo tunavitaka, vyama hivyo viwachague wanawake wenye uwezo wa kisiasa na wa uongozi.
Tunapenda kuvipongeza vyama vya siasa ambavyo vimetoa nafasi za wanawake kugombea nafasi za udiwani na ubunge na hata urais katika kura za maoni.
“Mwaka huu wanawake wengi wamejitokeza. Tungependa kuviomba vyama vya siasa kuhakikisha kuwa wale wanawake wenye uwezo wasimamishwe kugombea nafasi hizo na tunawaomba wananchi wote kuwachagua wanawake waliosimamishwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani, na wengine wapewe nafasi za teuzi mbalimbali Mkurugenzi wa GPF , Martha Nghambi.
Tunavikumbusha vyama kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake ambao hawakupata nafasi mwaka huu ili waweze kusimama na kugombea chaguzi zijazo ndani ya vyama vyao, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kadhalika tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, hawapendani badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii.
Kauli hizi za kuwa wanawake hatupendani si za kweli bali zimekuwa zikitumika katika jamii kuwagawa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, Reuben
Tunatarajia kuwa serikali, wadau wa siasa, vyombo vya usalama vitazingatia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK John Pombe Magufuli ya kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa wanawake katika uchaguzi mkuu na katika nafasi za uongozi na maamuzi. Pia tunampongeza kwa kuendelea kumchagua Mama Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu ujao.

Tungependa kumalizia kwa kusisitiza kauli zilizotolewa na Rais, viongozi wa vyama mbali mbali na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni huru, haki na wa amani.
Tunawakumbusha wagombea wote kuhakikisha kuwa hawatoi kauli zozote za uvunjifu wa Amani, kuchochea vurugu, kuwagawa watu kwa dini au makabila yao au matusi na udhalilishaji wa kijinsia kwa wagombea wengine.
Wakati huo, TAMWA, WiLDAF na GPF inaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea kuhimiza uchaguzi huru, wa haki na usawa na kutengenezwa kwa mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2020.

Rose Reuben Mkurugenzi Mtendaji – TAMWA
Anna Kulaya Mkurugenzi – WILDAF
Martha Nghambi Mkurugenzi – GPF

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WANAFUNZI 500 WAPEWA MBINU WASILOWEE KWENYE MADAWA YA KULEVYA.

Na Tonie kaisoe ,Arusha Wanafunzi zaidi ya 500 wa shule ya Sekondari Arusha Jiji na Wilaya ya Arumeru wamepewa mbinu

Read More...

MR. IBU AFARIKI DUNIA

Mchekeshaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria, John Okafor, almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Read More...

POLISI, LATRA WAPIGA FAINI MABASI YALIYO ZIDISHA NAULI ARUSHA.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu