Rais mpya wa Marekani Joe Biden amewaondolea raia wa Tanzania vikwazo vya kushiriki bahati nasibu ya viza, mwaka mmoja baada ya kutangazwa kwa vikwazo hivyo.
Januari 30, 2020 serikali ya Donald Trump ilitangaza kuwawekea Watanzania vikwazo vya kushiriki bahati nasibu hiyo pamoja na raia wa nchi nyingine kadhaa.
Kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa utawala uliopita wa Trump, nchi hizo ziliwekewa marufuku hiyo kwa kushindwa kufikia kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa.
“Nchi hizi, kwa sehemu kubwa, zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbali mbali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka,” aliyekuwa Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani Chad Wolf aliwaambia wanahabari baada ya kutangazwa kwa vikwazo.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetangaza kuwa marufuku hiyo imefutwa rasmi na rais mpya wa nchi hiyo Joe Biden aliyeingia madarakani juzi Jumatano.
“Mojawapo kati ya hatua zake za mwanzo kabisa akiwa Rais, Rais Biden ameondoa kikwazo kilichowekwa kwa Watanzania kuomba Viza ya Bahati Nasibu (Diversity VISA – DV),” ubalozi huo umeandika kupitia ukurasa wake wa Twitter