Tozo, ada kero 21 kwa wakulima zafutwa.

In Kitaifa

SERIKALI imetangaza kufuta tozo na ada 21 zilizoonekana kuwa kero kwa wakulima ama vikwazo kwa maendeleo ya Sekta ya Kilimo.

Hizo ni miongoni mwa ada na tozo zilizoonekana kuwa kero na kikwazo kwa maendeleo ya kilimo nchini mwaka jana wa fedha wakati serikali ilipofuta ada na tozo 78 kati ya 139. Pia imetangaza maeneo manne ya kuleta mageuzi ya kilimo na maisha ya wakulima nchini kuelekea uchumi wa viwanda na kipato cha kati. Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alibainisha nafuu na mikakati hiyo kwa wakulima jana bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/19. Ameomba kuidhinishiwa Sh 170,273,058,000. Waziri huyo alitaja ada na tozo hizo zinazofutwa katika tasnia ya sukari ni ada ya leseni ya kuuza nje ya nchi molasses ya Sh 500,000.

Katika tasnia ya chai ni ushuru wa chai ambayo hutozwa dola za Marekani 0.0125 kwa kilo, kwa kampuni ambazo huingiza chai kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuchanganya na chai ya ndani. Pia mchango kwa ajili ya utafiti wa zao la chai Sh 9.50 kwa kilo moja ya chai kavu na tozo kwa ajili ya mkutano wa wadau wa Sh mbili kwa kilo moja. Katika tasnia ya kahawa, ni makato ya asilimia 0.375 ya bei ya kahawa mnadani kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa kahawa, mchango kwa ajili ya Mfuko wa Kahawa unaochangiwa na wazalishaji na wanunuzi kwa kiwango cha asilimia 0.1 ya mauzo ya kahawa. Dk Tizeba alisema kwenye tumbaku kunafutwa mchango kwa ajili ya utafiti wa tumbaku wa Dola za Marekani 0.002 kwa kilo unaolipwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na leseni ya kuagiza tumbaku mbichi nje ya nchi cha asilimia 0.25 ya gharama ya kuagiza.

Kwa upande wa pamba, tozo iliyofutwa ni mchango kwa ajili ya maendeleo ya zao la pamba, fedha ambazo huwekwa kwenye mfuko wa maendeleo wa zao hilo kwa ajili ya kusaidia kutoa mbegu na dawa ambayo ni Sh 30 kwa kilo. Alisema tozo zitafutwa kwenye uzalishaji wa mbegu ambayo ni ada ya kwa ajili ya cheti cha usajili na utambuzi kwa muuza mbegu kwa Sh 100,000 na Dola za Marekani 50 na kufutwa ada ya cheti cha usajili wa aina za mbegu cha Sh 50,000 au Dola za Marekani 25. Ada nyingine iliyofutwa ni kwa ajili ya cheti cha majaribio ya mbegu kwa kiwango cha Sh 5,000 na Dola za Marekani mbili, ada ya cheti cha majaribio ya DUS ya Sh 5,000 au Dola za Marekani mbili na ada ya kuthibitisha nakala ya cheti ya Sh 2,500 au Dola za Marekani moja.

Waziri huyo alisema katika kuimarisha maendeleo ya ushirika, wizara yake itafuta tozo sita ambazo ni ada za utoaji wa barua ya kutambua chama cha ushirika cha awali cha Sh 20,000, utoaji wa cheti cha usajili na masharti kwa chama cha ushirika cha msingi Sh 50,000 na ada ya utoaji wa cheti cha usajili na masharti kwa chama cha ushirika cha upili Sh 100,000. Pia ada ya utoaji cheti cha usajili na masharti kwa chama kingine cha ushirika cha kati cha Sh 200,000, ada ya utoaji cheti cha usajili na masharti kwa shirikisho kwa kiwango cha Sh milioni moja na ada ya utoaji cheti cha usajili na masharti kwa uweekezaji wa pamoja kwa kiwango cha Sh 100,000.

Alisema Wizara ya Kilimo imewasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi na tozo kwa lengo la kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji na uendeshaji biashara katika shughuli za kilimo. Alisema ili kuboresha upatikanaji wa masoko ya mazao ya chakula hususani mahindi, serikali itaanzisha utoaji wa vibali kwa njia ya kielektroniki hivyo waombaji hawatalazimika kwenda Makao Makuu ya Wizara ya Kilimo.

Maeneo 4 ya mageuzi ya kilimo Maeneo hayo manne yalitangazwa na Waziri Tizeba bungeni jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/19. Ameomba kuidhinishiwa Sh 170,273,058,000. Alitaja maeneo hayo kuwa ni kuongeza uzalishaji na tija katika shughuli za wakulima na kusimamia kikamilifu hifadhi na matumizi jadidifu ya maji, ardhi na mazingira sambamba na kuongeza miundombinu ya umwagiliaji. Pia kuweka msukumo katika mabadiliko ya fikra na mazingira ya kibiashara kwa sekta ya kilimo kwa lengo la kubadili mtazamo wa uendeshaji kilimo kama shughuli ya kujikimu na badala yake iendeshwe kibiashara kwa faida ya nchi na wakulima.

Waziri Tizeba alisema katika mwaka 2018/19, viuatilifu aina ya Sulphur pamoja na vifungashio vya korosho korosho(magunia) havitatolewa kwa njia ya ruzuku kama ilivyokuwa msimu wa mwaka 2017/18. Wakulima watauziwa kwa bei itakayotangazwa na Bodi ya Korosho. Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeitaka serikali kupandisha bajeti ya wizara ya Kilimo hadi kufikia asilimia 10 ya bajeti ya serikali tofauti na sasa imekuwa ikishuka kila mwaka.

Akisoma maoni ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Christine Ishengoma alisema mwaka wa 2010/2011 bajeti ya wizara hiyo ilikuwa asilimia 7.8 ya bajeti ya serikali, mwaka 2011/2012 ilikuwa asilimia 6.9, mwaka 2016/2017 ni asilimia 4.9 na mwaka 2017/2018 ilishuka hadi asilimia 4.8 ya bajeti ya serikali. Kwa upande wa kuongeza uzalishaji wa sukari, kamati hiyo imependekeza kuwepo mkakati wa kuwezesha wakulima wadogo wa miwa kuzalisha miwa katika maeneo yao na kuwezeshwa kujenga viwanda vidogo ambavyo vitaongeza upatikanaji wa sukari hivyo kukabiliana na upungufu uliopo.

Kuhusu upungufu wa mafuta ya kula, kamati hiyo imeishauri wizara hiyo kuchukua hatua za makusudi na kutumia fursa ya soko la ndani kwa kuweka mipango na mikakati ya kuwezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kujenga viwanda vya kukamua alizeti. “Hatua hii itapunguza na kuokoa fedha nyingi zinazoagiz amafuta ya kula nje. Asilimia 70 ya mafuta ya kula nchi yanaagizwa kutoka nje na hugharimu Sh bilioni 413,”alisema. Akichangia, Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), amewahamasisha wabunge wanaotoka katika mikoa inayolima pamba, wasiunge mkono bajeti ya wizara hiyo kwa sababu haiwakomboi wakulima wa pamba.

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WANAFUNZI 500 WAPEWA MBINU WASILOWEE KWENYE MADAWA YA KULEVYA.

Na Tonie kaisoe ,Arusha Wanafunzi zaidi ya 500 wa shule ya Sekondari Arusha Jiji na Wilaya ya Arumeru wamepewa mbinu

Read More...

MR. IBU AFARIKI DUNIA

Mchekeshaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria, John Okafor, almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Read More...

POLISI, LATRA WAPIGA FAINI MABASI YALIYO ZIDISHA NAULI ARUSHA.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu