Umoja wa Afrika (AU) umemchagua Mwenyekiti mpya wa mwaka. Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amechukua wadhifa huo kutoka kwa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wakati wa mkutano wa viongozi wakuu na serikali mjini Addis Ababa.
Kikao cha 34 cha kumchagua mwenyekiti huyo kilifanyika siku ya Jumamosi huku kauli mbiu ikiwa ni “Sanaa, Utamaduni na Urathi, lakini masuala sugu yanaendelea kutawala mkutano huo unaokamilika leo Jumapili tarehe 7 mwezi wa Februari 2021.
Tshisekedi alichaguliwa katika kikao cha 2020 kuwa Mwenyekiti wa mwaka 2021, wadhifa unaozunguka miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama kwa kipindi cha mwaka mmoja. Tangu mwaka jana Tshisekedi amekuwa kwenye kampeni ya kujijenga kwa kufanya ziara kadhaa barani humo na kujiimarisha kidiplomasia.