Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas ametangaza jana kuwa uchaguzi wa Palestina uliopangwa kufanyika mnamo Mei 22 umeahirishwa kwa muda usiojulikana.
Abbas ametoa tangazo hilo baada ya mkutano na wawakilishi wa makundi kadhaa ya wapalestina mjini Ramallah na kusema uchaguzi huo hautafanyika hadi serikali yake itakapopata hakikisho kuwa eneo la Jerusalem Mashariki pia litashiriki kupiga kura.
Duru kutoka Palestina zinasema uamuzi huo unatokana na Israel kushindwa kuridhia matakwa ya mamlaka za Palestina za kuruhusu upigaji kura kufanyika pia kwenye eneo hilo la mji wa Jerusalem ambalo linakaliwa kwa mabavu. Kundi la Hamas ambalo linatawala ukanda wa Gaza ulio sehemu ya mamlaka ya ndani ya Palestina limesema halikubaliani na uamuzi wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo ambao ungekuwa wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 15.