PARIS,Bunge la Ufaransa leo hii limeridhia muswada ambao utafanya chanjo ya Covid-19 kuwa ya lazima kwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na takwa la kuviongezea nguvu vithibitisho vya afya kwa maeneo ya kijamii ya wazi.Hatua hiyo inaridhiwa wakati Ufaransa ikikabiliana na wimbi la nne la maambukizi ya virusi vya corona. Tayari wanaohudhuria katika majumba ya makumbusho, sinema au mabwawa ya kuogelea wanazuiwa kuingia katika maeneo hayo kama hawataonesha vithibitisho vya kupata chanjo ya Covid-19 au kufanya vipimo vya karibuni kabisa dhidi ya virusi vya corona.Vithibitisho hivyo kwa kiwango kikubwa vinahitajika katika matamasha au katika vilabu vya starehe. Lakini kwa sasa kuanzia mwezi ujao wa Agosti, nyaraka hizo zitahitajika zaidi katika kuingia katika migahawa, baa, na pia kwa safari za muda mrefu za treni na ndege.Kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Ulaya, Ufaransa ipo katika makabliano na kizazi kingine cha virusi vya corona aina ya Delta ambacho kinaambukiza kwa kwa kasi. Kirusi hicho ambacho kimegudulika kwa mara ya kwanza nchini India, kinatishia kuongeza muda zaidi wa makabiliano ya janga la corona na kufifisha jitihada za mataifa katika kufufua uchumi.