Wahalifu wa kimtandao wamedukua tovuti za serikali inayodhibitiwa na jeshi nchini Myanmar hii leo, wakati kukiibuka mzozo wa kimtandao baada ya mamlaka kufunga mawasiliano ya intaneti kwa siku ya nne mfululizo. Kundi hilo linalojiita “Wadukuzi wa Myanmar” walivamia tovuti kadhaa za serikali zikiwa ni pamoja na za Benki Kuu, ukurasa wa kijeshi wa propaganda, shirika la utangazaji la serikali, MRTV, mamlaka ya bandari na mamlaka ya chakula na dawa. Kupitia ukurasa wao wa Facebook, wadukuzi hao wamesema wanapigania haki nchini Myanmar. Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya maelfu ya watu kuandamana kote nchini Myanmar kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyuiangusha serikali ya kiraia ya Aung San Suu Kyi mapema mwezi huu.
