Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wamefungua rasmi mashtaka bungeni dhidi ya Rais Donald Trump kwa lengo la kutaka kumuondoa madarakani wakimtuhumu kwa kuchochea uvamizi wa majengo ya bunge Capitol Hill wiki iliyopita mjini Washington.Hapo jana, Wademocrat waliwasilisha azimio katika Baraza la Wawakilishi kumtaka makamu wa rais Mike Pence kutumia ibara ya 25 ya katiba ya nchi hiyo kumtimua Trump madarakani kwa msingi kuwa hafai kuwa ofisini.Lakini wabunge wa chama cha Republic walizuia azimio hilo kupitishwa moja kwa moja, na ndipo Wademocrat wakawasilisha mashtaka ya uchochezi dhidi ya Trump.Hatua hiyo inayolenga kuyazima matarajio ya siku za baadaye ya Rais Trump kujihusisha katika siasa, inaweza kuwa kilele cha kile kimekuwa miaka minne ya malumbano kuelekea kuapishwa kwa Joe Biden kuwa rais mpya Januari 20.
