Kwa mujibu wa makubaliano yaliyotangazwa siku ya Ijumaa (23 Novemba) mjini Nairobi, Kenya, sasa Felix Tshisekedi anayeongoza chama kikubwa zaidi cha upinzani cha UPDS atasimama kwa niaba ya chama chake na kile cha spika wa zamani, Vital Kamerhe.
Uamuzi huu umefikiwa ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya uchaguzi wa tarehe 23 Disemba kwenye taifa hilo tajiri kwa madini la Afrika ya Kati.
Tangazo hili linamaanisha kwamba uchaguzi huu utakuwa na pande tatu kuu zinazowania: Emmanuel Ramazani Shadary anayeungwa mkono na Kabila, Martin Fayulu anayeungwa mkono na viongozi wawili wakuu wa upinzani waliozuiwa kuwania urais – Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi, na Tshisekedi anayeungwa mkono na Kamerhe.