Watu wasiopungua 30 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 200 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama kwenye ziwa huko magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Meya wa mji wa Inongo Simon Mboo Wemba, amelieleza shirika la habari la AFP kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 350, na kwamba watu waliookolewa ni 182 pekee. Ajali hiyo ilitokea usiku wa Jumamosi katika ziwa Mai-Ndombe. Wemba ameongeza kwamba imekuwa vigumu kuhesabu idadi kamili ya abiria kwasababu wengi wanahofiwa kuwa wahamiaji haramu. Usafiri wa mito na maziwa ni moja ya usafiri unaotumiwa sana nchini Congo. Mwezi uliopita kiasi ya watu 167 walifariki katika ajali mbili tofauti za majini na kumfanya rais Felix Tshisekedi kutoa amri ya kila abiria kufaa jaketi la uokozi.