Zitto Kabwe Kupeleka Mpango Mbadala wa Bajeti Bungeni

In Kitaifa, Siasa
Kiongozi  wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema amejipanga kupeleka bungeni mpango mbadala kuhusu sera za kibajeti akidai mpango wa bajeti ya serikali umejikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu.
Zitto (41), ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mrejesho wa ziara yake aliyoifanya katika kata zinazoongozwa na chama chake, nchini kote.
Alisema mpango wake huo umelenga kuunda mpango mwingine mpya utakaosimamia masuala ya uchumi shirikishi unaozalisha ajira pamoja na kuhakikisha kilimo na viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo vinapewa kipaumbele.
Vitu vingine ambavyo alisema vinapaswa kupewa kipaumbele ni usalama wa chakula na lishe pamoja na huduma bora za kijamii hususani maji, elimu na afya.
“Juzi serikali imeainisha vipaumbele vya kibajeti kwa mwaka 2018/19. Masuala ya watu hususani kilimo, maji hayamo kwenye vipaumbele hivyo,” Zitto alisema na kufafanua zaidi:
“Ni rai yetu kwa serikali ijitazame katika eneo hilo, ikae chini na kuja na mpango mpya utakaojikita katika masuala ya watu na siyo kama mpango huu wa sasa unaojikita kwenye vitu tu.
“ACT-Wazalendo tutahakikisha tunaupinga bungeni mpango huu wa bajeti wa sasa ili uandaliwe upya kwa sababu huu uliopo unawaacha kando kwa asilimia 70 Watanzania, tunataka tuwe na ‘balance’ (uwiano) ya vipaumbele vya kujenga nchi na vya kujenga taifa ili tuhakikishe vitu vya muhimu kama elimu, kilimo, afya na vitu vingine vinavyowahusu watu moja kwa moja vinaguswa na kupewa kipaumbele.”
Wiki iliyopita serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk, Philip Mpango iliwasilisha kwa wabunge mapendekezo yake kuhusu ukomo wa bajeti na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/19.
Dk. Mpango alisema bajeti ijayo ambayo itakuwa ya tatu kwa serikali ya awamu ya tano inatarajia kuwa Sh. trilioni 32.476. Kati yake, Sh. trilioni 20.468 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 63 ya bajeti na Sh. trilioni 12.007 zitatumika kwa shughuli za maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti.
Waziri huyo alisema miradi kielelezo itakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge kiasi cha Sh. trilioni 1.4, kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege ya pili aina ya Dreamliner-Boeing 787, ununuzi wa ndege moja mpya aina ya Bombadier Dash 8 Q400 na kuanza uendeshaji wa ndege mpya Boeing 787 na Bombardier CS 300, zikitengewa Sh. bilioni 495.6.
Pia alisema Sh. bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa na ujenzi wa njia kuu za kupitishia maji katika mradi wa Stieglers’ Gorge.
Katika mkutano wake na waaandishi wa habari jana, Zitto ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), pia aliiomba serikali kuitisha mkutano wa kitaifa wa maridhiano ya kisiasa kama jukwaa la kuzijadili changamoto za uendeshaji wa siasa nchini.
Alisema mkutano huo utasaidia kuondoa uadui unaoendelea kukua kwa sasa kati ya serikali na wananchi, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za wanafunzi pamoja na vyama vya upinzani na anaamini mazungumzo ya kitaifa ndiyo jambo sahihi la utatuzi wa suala hilo.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo huyo pia alipendekeza kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza matukio ya mauaji, utekwaji na kupotea kwa wafanyabiashara, viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari pamoja na wananchi wengine.

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WANAFUNZI 500 WAPEWA MBINU WASILOWEE KWENYE MADAWA YA KULEVYA.

Na Tonie kaisoe ,Arusha Wanafunzi zaidi ya 500 wa shule ya Sekondari Arusha Jiji na Wilaya ya Arumeru wamepewa mbinu

Read More...

MR. IBU AFARIKI DUNIA

Mchekeshaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria, John Okafor, almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Read More...

POLISI, LATRA WAPIGA FAINI MABASI YALIYO ZIDISHA NAULI ARUSHA.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu