Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2017/2018, huku ikisisitiza kuwa hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi kwa ujumla ni shwari licha ya kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya nchi ,za ukanda wa Afrika Mashariki maziwa makuu na pembe ya Afrika.

Akiwasilisha bajeti jana  bungeni mjini Dodoma waziri wa wizara hiyo dokta HUSSEIN MWINYI, ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Somalia na Sudan Kusini.

Amesema uwepo wa hali ya matishio ya ugaidi wa kimataifa ulivilazimu vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana,na nchi jirani na raia wake kuendelea kuwa katika hali ya tahadhari na umakini ili endapo kutajitokeza dalili yoyote inayotishia usalama, hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

Akizungumzia vitendo vya uhalifu dokta MWINYI amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo wizara kupitia Jeshi la Wananchi la Tanzania(JWTZ), imeendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na mataifa mengine katika kupambana na matishio ya kiusalama yakiwemo ugaidi, uharamia na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ADADI RAJABU ameishauri serikali kulipatia fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge fungu 38, Ngome ambalo linahusika na mambo ya msingi kwa uwepo wa nchi na kwa kuwa kasma za matumizi muhimu zipo katika fungu hilo.

 

Wizara hiyo imeomba kiasi cha shilingi  trilioni 1.725 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo ili iweze kutekeleza majukumu yake.

Exit mobile version