Mchezaji wa Klabu ya Mabingwa watetezi wa Ligi kuu Bara Yanga SC Ibrahim Ajibu amesema matokeo yasiyoridhisha wanayoyapata hivi sasa, ni sehemu ya mchezo, hivyo mashabiki waendelee kuwaunga mkono.
“Mashabiki watulie na waendelee kutuunga mkono ili tuweze kufanya vizuri kwenye mechi zijazo kwa sababu haya matokeo hata sisi hatuyafurahii.
“Matokeo yetu dhidi ya Singida ni sehemu ya mchezo, tulijitahidi sana kuhakikisha tunapata ushindi lakini haikuwa hivyo kwa sababu na wenzetu nao walijipanga, kikubwa ifahamike wazi kwamba, ligi bado mbichi,” amesema Ajibu.
Yanga imepata sare ya pili mfululizo huku mashabiki wake wakionyesha kutofurahishwa baada ya kikosi chao kuomba mechi iishe mapema wakati Singida United walipokuwa wakishambulia kama nyuki.
Yanga na timu nyingine zina nafasi ya kujiandaa kwa kipindi hiki kutakuwa na mapumziko wakati wa kalenda ya Fifa, hivyo ni nafasi nyingine kuyafanyia kazi makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza.
