Shirika la kimataifa linalohusika na utetezi wa haki za binadamu la Amnesty International limesema uchaguzi wa Rais wa Rwanda utakaofanyika mwezi ujao ambao pia Rais wa sasa Paul Kagame atakuwa anawania muhula wa tatu wa uongozi utafanyika katika mazingira ya hofu.
Kwa mujibu wa Amnesty uchaguzi huo utakaofanyika August .4 utafanyika huku kukiwa na rekodi kwa wanasiasa wa upinzani nchini humo kudhibitiwa, waandishi wa habari pamoja na wanaharakati kutiwa magerezani, kuuawa na wengine kulazimika kuikimbia nchi hiyo.
Rais wa Rwanda Paul Kagame amekuwa Rais wa nchi hiyo tangu wakati kundi lake la waasi lilipokomesha mauaji ya halaiki nchini humo ya mwaka 1994.
Hadi sasa ni mgombea mmoja tu wa upinzani , Frank Habineza aliyepitishwa na tume ya uchaguzi nchini humo kushindana na Rais Kagame katika uchaguzi huo. Wagombea wengine akiwemo mwanamke mmoja bado wanasubiri hatima yao ya kupitishwa na tume hiyo.
