Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewataka Waislamu kujiepusha na mtu anayejiita mtume na kufundisha mambo yanayopingana na Imani ya Kiislamu, eneo la Kibaha Misugusugu mkoani Pwani.
Akizungumza kwa niaba ya Mufti Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Mufti, Shehe Khamis Mataka amesema Hamza Issa ndiye anayedai kushukiwa na roho ya Nabii Illyasa na kuwaaminisha watu kwenye mafundisho yake kuwa yeye ndiye Nabii Ilyasa.
Amesema baada ya kupokea maazimio ya Baraza la Mashehe wa Mkoa wa Pwani kuhusu taarifa za Hamza Issa kujiita mtume, Mufti Zubeir alikaa na Baraza lake la Ulamaa na kupitisha maazimio mbalimbali ikiwemo kuwaonya Waislamu, kuwa yeyote atakayemfuata Hamza Issa, atakuwa ametoka ndani ya Uislamu.
Shehe Mataka alitaja maazimio mengine yaliyopitishwa na Baraza la Ulamaa ni pamoja na kuwataka mashehe wa mikoa, wilaya na Maimamu, kutompa nafasi Hamza Issa ya kuzungumza misikitini wala kusikiliza CD zake ,ili kutoruhusu upotoshaji wake kuenea katika jamii.
Msemaji huyo wa Mufti alieleza kuwa Baraza la Ulamaa ni chombo cha kuchunga nidhamu ya dini katika Uislamu na kuongeza kuwa mafundisho yanayotolewa na Hamza Issa, kuhusu kuingiwa na roho ilyomfanya kuwa mtume ni mara ya kwanza kusikika duniani kwa mujibu wa Imani ya Kiislamu.
