Baraza la Seneti la Marekani kwa sauti moja hapo jana limepitisha mswada wa kuziwekea vikwazo vipya Urusi, Iran na Korea Kaskazini, na kuuwasilisha mswada huo kwa Rais Donald Trump ambaye sasa anatakiwa kufanya uamuzi wa kutia saini ili ugeuke kuwa sheria.
Mswada huo unamzuia rais Trump kuipunguzia vikwazo Urusi bila ya idhini ya seneti.
Trump amekuwa akisisitiza mara kwa mara juu ya kuwepo kwa uhusiano mzuri na Urusi, licha ya uchunguzi uliofanywa mara kadhaa kuhusu Urusi kuingilia uchaguzi wa rais wa mwaka jana uliomuweka Trump madarakani.
Vikwazo dhidi ya Korea ya Kaskazini vinalenga silaha zake za nyuklia na mpango wake wa makombora na Iran inalengwa kwa shughuli zake za kigaidi, ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na mipango ya makombora ya masafa marefu.
