Benki ya Dunia yajipanga kukuza uchumi wa Tanzania na kupunguza umasikini

In Kitaifa, Uchumi
Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Bi. Bella Bird ametoa kauli hiyo leo tarehe 04 Desemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kubainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu hususani barabara na reli, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na elimu kwa kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu inaongezeka.
Maeneo mengine ni kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa maji, usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia masikini.
Bi. Bella Bird amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Benki ya Dunia na amemuahidi kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingine.
“Mwaka uliopita Benki ya Dunia imetoa mikopo nafuu yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.2 (Shilingi Trilioni 2.7) kwa Tanzania, fedha hizi zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa miradi hiyo inakwenda vizuri na wananchi wanafurahia, kwa sasa tunapanga namna tutakavyotoa mikopo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo katika kipindi kijacho” amesema Bi. Bella Bird.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake na Tanzania katika maendeleo na amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali itazisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na benki hiyo ili zilete matokeo yanayotarajiwa.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa maeneo yote ambayo benki hiyo imeyataja kuwa kipaumbele katika fedha zitakazotolewa kuanzia sasa ni muhimu kwa ustawi wa Tanzania na amesisitiza kuwa fedha zitakazotolewa kwa mkopo zielekezwe katika maendeleo na sio vinginevyo.
“Naishukuru sana Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono, nitafurahi kuona mnaendelea kutupatia fedha ambazo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kuleta manufaa mapana na endelevu, badala ya kugawa fedha kwa watu na baadaye nchi inakuja kuzilipa kwa kukusanya kodi za wananchi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli leo ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Desemba, 2017

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

Viwango vya maadili kwa viongoiz yaongezeka.

Imeelezwa kuwa viwango vya uzingatiwaji wa maadili kwa viongozi na watumishi wa umma nchini,vimeongezeka hadi kufikia asilimi 75.9 kwa

Read More...

Watu 193 wawekwa karantini kisa virusi vya Marburg.

Mganga Mkuu wa serikali Dkt Tumaini Nagu,amesema hakuna kisa kipya kilichoongezeka kuhusu vifo vilivyosababishwa na virusi vya Ugonjwa wa

Read More...

SERIKALI YAFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi na uchukuzi,isemema kuwa katika kuhakikisha wanakuwa na Taarifa za uhakika za Hali ya hewa

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu