SERIKALI kupitia Maraisi wa Vyama vya Ushirika imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu wa fedha na mali za vyama hivyo nchini ,baada ya kuvunja bodi 10 za vyama hivyo vya wakulima wa korosho wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Aidha, makatibu wakuu 10 wa vyama hivyo wameondolewa madarakani, na bodi mpya za muda zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika.
Kaimu Mrajisi Msaidizi, Revocatus Nyagilo ambaye ameongoza vikao vya kuvunjwa bodi hizo kwa niaba ya mrajisi wilayani Nachingwea, amesema hatua hiyo inatokana na uchunguzi uliofanywa na Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), kwa kushirikiana na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO).
Nyagilo amesema uchunguzi huo uliofanyika mwaka jana, ulibaini ubadhirifu wa mabilioni ya fedha na mali, katika vyama hivyo katika mikoa ya Lindi na Mtwara na hivyo kuamua kuitisha mikutano maalum ya vyama hivyo, katika mikoa hiyo kwa hatua zaidi.
Katika taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi hiyo wilayani Nachingwe imeeleza kuwa ,vyama ambavyo bodi zake zimeondolewa madarakani na makatibu kuvuliwa nafasi zao Aprili 20 mwaka huu kwa ubadhirifu ni Ndomondo, Naipanga, Chiumbati, New Stesheni na Mchonda.
Vingine ni Makina, Mkotokuyana, Nache, Namikango na Ndanga limbo,Vyote 10 ni Vyama vya Ushirika vya Mazao na Masoko (AMCOS) na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
