Chama cha ACT-Wazalendo kimemvua uenyekiti wa chama hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kufuatia uteuzi wake.
Uamuzi huo umetangazwa leo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samsoni Mwigamba alipofanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mwigamba alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kuwa kutokana na uteuzi huo, Mghwira hawezi kufanya kazi ya uenyekiti wa chama hicho kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa chama amesifia uamuzi wa Rais John Magufuli kuwateua watu kutoka upande wa upinzani, lakini ameomba kamati ya uongozi kumshauri kuweka mfumo bora wa kufanya uteuzi kutoka upande wa upinzani ili kuepusha migongano.
Mama Mghwira aligombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu uliopita kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo.
