Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kanda ya kati kimeitaka serikali kuwalipa fidia wakazi wa Manispaa ya Dodoma ambao kwa namna moja au nyingine wameathirika na vitendo vya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa kuwapora ardhi yao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Mafunzo na oganaizesheni wa Chadema, BENSON KIGAILA wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma.
Amesema kuwa Rais hawezi kuivunja CDA na ikawa ndiyo mwisho wake bila kuangalia madhara yaliyosababishwa na mamlaka hiyo ,kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka 44 iliyofanya kazi.
Mbali na hilo aliwapongeza wakazi wa Manispaa ya Dodoma pamoja na viongozi wao, kwa kupaza sauti kwa nguvu dhidi ya uonevu uliokuwa unafanywa na CDA na hatimaye kupelekea Rais kuivunja rasmi.
CDA ilianzishwa kwa amri ya Rais, Aprili mosi, mwaka 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 na kuvunjwa Mei 15, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali.
