Christian Democratic Union CDU kimekishinda chama cha Social Democrats SPD katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia ambayo ni ngome ya SPD.

Chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU kimekishinda kile cha Social Democrats SPD katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia ambayo ni ngome ya SPD.
Matokeo ya awali yanaonyesha CDU kimeshinda uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili kwa asilimia 33 huku SPD ambacho kimeliongoza jimbo hilo kwa karibu nusu karne kikiibuka katika nafasi ya pili kwa asilimia 31.3 na chama cha Free Democratic Party FDP kinachonuia kurejea katika bunge la Ujerumani kikiwa katika nafasi ya tatu kwa asilimia 12.5 ya kura.
Ushindi huo wa CDU umeongeza matumaini ya Merkel kusalia madarakani kwa muhula wa nne katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Septemba mwaka huu.
Mgombea Ukansela wa SPD Martin Schulz amesema matokeo hayo ni pigo kubwa kwa chama chake na kwake binafsi.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Schulz amesema wameshindwa vibaya katika jimbo analotokea. Asilimia 65. 2 ya watu walio na haki ya kupiga kura walishiriki uchaguzi huo.

Exit mobile version