Baada ya kuwa nje ya uwanja kwa takriban mwezi mzima mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ndombo Ngoma amerejea kwenye kikosi hicho na yupo fiti kucheza mbele ya Waarabu MC Alger ya Algeria kwenye mechi ya Kombe la shirikisho
Daktari wa Yanga, Edward Bavu amesema Ngoma ana asilimia 100 za kucheza mchezo huo kwani yuko fiti na kwamba ana zaidi ya wiki mbili tangu apone ambapo alikuwa akifanya mazoezi madogo madogo na timu.
“Sina shaka tena na hali ya Ngoma ambaye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu tayari amesharejea uwanjani na kwamba ana uhakika wa kuwavaa MC Alger kesho kwani hali yake kwa jumla inaridhisha sana na kwamba amepata muda mrefu wa kufanya mazoezi na wenzake.” Alisema Bavu
Ngoma amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara tangu ulipoanza mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu Tanzania Bara kiasi cha kumfanya ashindwe kuitumikia klabu yake ya Yanga kwenye michezo muhimu mbalimbali iliyokuwa mbele yao ukiwemo ule dhidi ya Simba ambao waliolala mabao 2-1.
