Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika, kuanza kutumia dawa mpya ya kupambana na virusi vya Ukimwi inayofahamika kama DTG.
Dawa hiyo mpya inayosaidia mwathirika kuendelea kuishi kwa muda mrefu, ilitengenezwa na kuidhinishwa na Marekani mwaka 2013.
Watalaam wamesema waathiriwa zaidi ya 20,000 nchini Kenya wanapewa dawa hiyo kuona matokeo yake na baadaye itakwenda nchini Nigeria na hatimaye nchini Uganda.
Doughtiest Ogutu, mmoja wa watumizi wa dawa hiyo mpya, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa ameamua kutumia hiyo mpya kwa sababu dawa nyingine aliyokuwa anatumia ilikuwa haimsaidii.
Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayoendelea kukabiliwa na janga la maambukizi ya Ukimwi.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na maambukizi ya Ukimwi UNAIDS, linalenga kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 90 ya waathiriwa wa virusi hivyo watakuwa wameanza kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
