Fenerbahce wanamtaka mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa.

Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki imefanya mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa kuhusu uwezekano wa kumchukua kwa mkopo.

Costa, 28, amesalia nchini Brazil na amekataa kurejea England.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania alishindwa kuhama kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi ya Premia kabla ya siku ya mwisho ya kuhama wachezaji katika ligi nyingi kuu Ulaya.

Hata hivyo, dirisha la uhamisho wa wachezaji Uturuki bado liko wazi na litafungwa baadaye leo Ijumaa.

Duru zinasema baada ya mazungumzo ya kwanza kufanyika, uwezekano wake kuhama ni finyu, lakini mazungumzo bado yanaendelea.

Costa ameambia na meneja wa Chelsea Antonio Conte ajitafutie klabu itakayomchukua.

Alitaka kurejea Atletico Madrid majira ya joto lakini klabu hiyo ya Uhispania hairuhusiwi kuwasajili wachezaji kutokana na marufuku waliyowekewa hadi Januari.

Hii ina maana kwamba Costa anaweza tu kuhamia klabu hiyo Januari mwakani.

Mshambuliaji huyo hajajumuishwa kwenye orodha ya wachezaji wa Chelsea watakaoshiriki Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Exit mobile version