Rais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Gianni Infantino, ameziandikia barua nchi 32 zitakazoshiriki katika michezo ya Kombe la Dunia nchini Qatar, kujikita katika michuano hiyo badala ya kuiburuta kandanda katika mizozo ya kisiasa na kiitikadi. Infantino amesema katika barua hiyo kwamba kila mtu atakaribishwa nchini Qatar bila kujali asili yake, imani yake ya kidini, jinsia, utaifa au tabia yake ya kimapenzi.
Kituo cha habari cha Sky News cha nchini Uingereza ambacho kimepata nakala ya barua hiyo, kimesema haielezi chochote kuhusu ombi la nchi nane za Ulaya, ambazo zilitaka manahodha wa timu zao wavae utepe wenye mchanganyiko wa rangi unaowakilisha haki sawa kwa wapenzi wa jinsia moja, kama jibu kwa sheria za Qatar zinazokataza ushoga. Watetezi wa haki za binaadamu pia wanakosoa rekodi ya Qatar ya haki za binadamu, hususan mazingira duni kwa wafanyakazi waliojenga viwanja vya michezo.
