Kundi la mataifa yaliyoendelea na yanayoinukia kiuchumi la G20 limeahidi kuepuka vizuizi vya kibiashara kwa bidhaa muhimu ikiwemo chakula wakati wote wa mzozo wa janga la virusi vya corona.
Ahadi hiyo imetolewa na mawaziri wa biashara na uwekezaji wa mataifa ya kundi hilo ambao wamesema vikwazo kwa usafirishaji wa vifaa vya matibabu na bidhaa muhimu havipaswi kulemaza biashara na mifumo ya usambazaji wa mahitaji duniani.
Mawaziri hao walishiriki mkutano kwa njia ya vidio pia wameahidi kujizuia kuweka vizuizi kwenye mazao ya kilimo pamoja na kuepuka kuweka akiba ya chakula isiyo ya lazima.
Hatua ya kundi la G20 inakuja baada ya shirika la fedha la kimataifa IMF na shirika la Biashara duniani WTO kuonya dhidi ya kuongezeka kwa vizuizi vya usafirishaji wa bidhaa unaotokana na janga la virusi vya corona.
