Tathmini mpya kuhusu ugonjwa wa Zika kwa nchi za Amerika ya Kusini imeonyesha kuwa athari za kijamii na kiuchumi zitokanazo na ugonjwa huo zitakuwa za muda mrefu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Ikifanywa kwa ushirikiano kati ya shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na shirikisho la msalaba na hilal nyekundu, IFRC, tathmini hiyo imeonyesha kuwa Zika itagharimu nchi hizo kati ya dola bilioni 7 hadi 18 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Brazil ndiyo itakayobeba mzigo zaidi kwa kuwa Zika inasababisha watalii kupungua na hivyo mapato ya kiuchumi kushuka.
Kwa kuzingatia athari mtambuka za Zika, serikali zimetakiwa kupanga bajeti zao ipasavyo badala ya kujikita tu katika kuimarisha huduma za afya na wakati huo huo kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa kama homa ya dengue, manjano na chikingunya ambayo yote huenezwa na mbu aina ye Aedes anayesambaza pia virusi vya Zika.
Katika kupanga bajeti, serikali zimetakiwa kujumuisha wadau mbali mbali ikwemo jamii, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.
