Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Amesema Serikali imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000, ambavyo bado havijaunganishiwa na nishati hiyo.
Amesema hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga, Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi.
Waziri mkuu amesema kuwa gharama za kulipa umeme huo ni shilingi elfu 27 tu, ambapo wananchi hawatawajibika kulipia nguzo na fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimebebwa na Serikali.
Amesema lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa, vitafungiwa umeme Jua (sola), hivyo kufungua fursa za Ajira na kukuza uchumi.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Lindi, Johnson Mwigune amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu, mkandarasi aliyepangwa kufanya kazi katika vijiji hivyo atakuwa ameanza kusambaza umeme.
