Serikali imesema kuwa itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo katika kutoa wataalam, kuandaa michoro na kusimamia ujenzi wa barabara zote zinazoingia katika viwanda vinavyojengwa mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa mara baada ya uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuandika barua kwa Wizara hiyo kuomba msaada wa kujengewa barabara ya Km 1 inayoingia kwenye kiwanda kipya cha Matunda cha Sayona kutoka kwenye barabara kuu ya Chalinze – Arusha na ile iliyopo katika kiwanda cha kutengeneza marumaru na masinki cha Twyford.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kutumia fedha za Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), kuona namna ya kujenga barabara hizo na kuhakikisha ubora wa barabara hizo unaendana na thamani ya fedha zinazotolewa.
Kuhusu ujenzi wa barabara inayoingia kwenye kiwanda cha kutengeneza marumaru na masinki kilichopo wilayani hapo, Naibu Waziri Ngonyani, ameuagiza uongozi wa TANROADS mkoani humo kupima na kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa barabara hiyo ili kupata taarifa sahihi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bw. Magid Mwanga, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya kazi kwa vitendo kwa kuchukua hatua za haraka za kutembelea maeneo hayo na kuboresha miundombinu ya barabara katika viwanda ili kuhamasisha na kuchochea wawekezaji wa viwanda nchini.
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga miundombinu bora kwa wananchi wake na Taifa kwa ujumla ili kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na huduma za usafirishaji ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
