Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo imeahirisha kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mmiliki wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL Harbinder Singh Sethi, na James Rugemarila hadi August 31 2017 kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha kuwa, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo ya wakili wa Swai, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi August 31 2017 ambapo washtakiwa wamerudishwa rumande.
Harbinder Singh Sethi pamoja na Mfanyabiashara James Rugemarila, kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya zaidi ya Bilioni 3.
