Hifadhi ya Pori la Akiba la Selous imepata ufadhili wa Sh bilioni 47.124 kutoka Ujerumani kwa ajili ya mradi wa miaka mitano wa Maendeleo ya Uhifadhi wa Ikolojia ya Pori la hifadhi hiyo (SECAD).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke alizindua mradi huo ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society).
Akizungumza katika hafla iliyofanyika jana, Matembwe Selous Mkoani Morogoro, Maghembe amesema Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya KFW ilichangia Euro milioni 18 (sawa na Sh bilioni 45.124) katika mradi huo wa miaka mitano huku mashirika ya WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society) kwa pamoja zikachangia Euro 400,000 (sawa na Sh bilioni 2).
Profesa Maghembe almesema,Mradi huu ni muhimu kwa kuwa utasaidia kuongeza nguvu kwenye jitihada za kuendeleza na kuimarisha hifadhi ya pori hili la Selous ikiwemo upatikanaji wa vitendea kazi pamoja na kutuongezea nguvu kwenye mapambano dhidi ya ujangili.
Alisema jitihada ambazo Serikali imeshazifanya katika pori hilo ni pamoja na kuimarisha doria za ndege zenye rubani na zisizo na rubani (drones), kutoa mafunzo ya jeshi usu kwa askari, kuongeza maaskari pamoja na vitendea kazi ambapo katika mwaka ujao wa fedha Serikali pia itatoa magari mengine 15 kusaidia pori hilo.
Akizungumzia changamoto ya ujangili katika pori hilo, alisema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo hilo ambapo majangili wengi wameshakamatwa katika maeneo ya Tunduru, Namtumbo na maeneo ya katikati ya Selous.
