Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC) imepiga marufuku wapigapicha ndani ya vituo vya kupigia kura, pia haitaruhusiwa kujipiga picha wakati wakipiga kura.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati, pia amepiga marufuku, wapigakura kupiga picha karatasi za kupigia kura wakionesha wamemchagua nani.
Ni waandishi wa habari pekee wenye vibali ndio watakaoruhusisiwa kupiga picha na kuandika habari za uchaguzi ifikapo siku ya uchaguzi Agosti 8, mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa katazo hilo limelenga kulinda haki ya mpiga kura kutunza siri yake kwa mujibu wa Sheria na kuzuia kushawishi wengine kumpigia kura kiongozi asiyemtaka.
