Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, leo amemuapisha Prof Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alimteua kushika wadhifa huo Septemba 10 mwaka huu.
Katika ghafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa wakiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Majaji wengine wa Tanzania.
Katika hotuba yake Rais Magufuli amezungumza mambo kadhaa, lakini pia kuhusu baadhi ya wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa, na kudai kuwa yeye anaogopa kusaini ili wafungwa hao wanyongwe.
Kwa upande wake Jaji Ibrahim Juma aliyeapishwa amesema anashukuru kwa kurasimishwa kushika wadhifa huo, ambao alikuwa ana ukaimu takriban miezi nane mpaka alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu.
Katika hotuba yake ya kwanza Jaji Mkuu Ibrahi Juma ameahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa weledi, ikiwemo kulinda sheria na kuweka imani kwa wananchi, kwani wao ndiyo watetezi wao.
Ibrahim Juma alianza kutumikia wadhifa wa Kaimu Jaji Mkuu tokea Januari 18 mwaka 2017, baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa nchi Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kustaafu.
