January Makamba apinga hoja ya Mbunge wa Mbarali Mkoani Mbeya.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira na Muungano), January Makamba amepinga hoja ya Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Haroun Mulla inayokinzana na azma ya serikali ya kuhifadhi na kurudisha ikolojia ya bonde la mto Ruaha Mkuu.

Katika mkutano uliofanyika mjini Iringa hivi karibuni ambao Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliutumia kuzindua kikosi kazi kitakachokuja na mapendekezo yatakayotumiwa kunusuru bonde hilo ambalo pia ni chanzo pekee cha maji cha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mulla alisema: “Nimetembea hifadhi mbalimbali duniani, wenzetu wamechimba mabwawa makubwa ya maji katika hifadhi zao.

Tanapa (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa) wanatakiwa kuiga nchi hizo, chimbeni mabwawa ya maji hifadhini kuongeza uhakika wa maji kwa wanyama.” Mbunge huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Highlands Estates inayomiliki moja ya mashamba makubwa ya mpunga wilayani Mbarali, alisema katika kushughulikia suala la bonde hilo, serikali inapaswa kuzingatia uwiano wa mapato yanayotokana na shughuli za kilimo na zile za uhifadhi.

Mulla amesema kilimo katika bonde hilo la Usangu kinatengeneza zaidi ya Shilingi  trilioni moja kwa mwaka, wakati shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zinatengeneza wastani wa Sh bilioni 4.5 kwa mwaka.

Akijibu hoja ya mbunge huyo, Waziri Makamba amesema suala la mazingira ni suala nyeti ambalo haliwezi kupimwa kwa kuangalia ni kiasi gani cha fedha kinapatikana katika eneo lenye manufaa mapana kwa taifa. “

Aidha amesema hali ya mazingira katika bonde hilo inazidi kuharibika na kusababisha athari zinazotishia ustawi wa jamii, mazingira, uchumi wa nchi na mifumo ya ikolojia ya bonde hilo

Amesema mto Ruaha Mkuu ni wa pili kwa ukubwa nchini baada ya Mto Rufiji ukiwa na urefu wa kilometa 475 na lindi maji lenye ukubwa wa kilometa za mraba elfu 68,000 inayojumuisha baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe.

Exit mobile version