Jeshi la Uganda limekanusha taarifa kuwa liko tayari kuingia nchini Kenya, kusaidia kudhibiti hali ya usalama baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini humo.
Katika uchaguzi huo rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, huku mpinzani wake mkuu Raila Odinga akiyapinga matokeo hayo.
Waziri wa mawasiliano nchini Uganda Frank Tumwebaze, amesema jeshi la Uganda haliwezi kutumwa nje ya nchi hiyo, kushiriki operesheni ya kijeshi kisiri.
Msemaji wa jeshi la Uganda Richard Karemire amesema kuwa, Kenya ni nchi huru na usalama wake umo chini ya serikali ya nchi hiyo.
Aidha amesema Uganda haijapokea ombi lolote kutoka kwa Kenya, kutuma majeshi yake nchini humo au kuomba usaidizi.
