JOPO la Madaktari bingwa kutoka Marekani, Hospitali ya Taifa ya Rufaa Muhimbili – MOI ya Dar es Salaam na Mount Meru ya mkoani Arusha ,wameendelea kuwafanyia matibabu kwa kina wanafunzi majeruhi watatu wa ajali ya Basi la Shule ya Lucky Vincent.
Mbali na uchunguzi huo wanafunzi hao watatu ambao kwa sasa wameendelea kuimarika, shughuli nyingine zilizofanyika jana zilikuwa ni kwa upande wa wazazi wa watoto na watoto wenye kujaza fomu, kwa ajili ya taratibu za Hati ya kusafiria.
Serikali kwa kushirikiana na jopo hilo la madakari bingwa kutoka Marekani, wameendelea na taratibu za kuwasafirisha majeruhi hao ambao ni Geofrey Tarimo, Sadia Awadhi na Doreen Mshanga, kwa ajili ya matibabu zaidi nchini Marekani.
Akizungumza mjini hapa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, aliyekuwa mwenyeji wa Madaktari waliotembelea jimboni kwake kisha kuelekea Ngorongoro amesema, taratibu zinaendelea za kuhakikisha watoto hao wanatibiwa.
Aidha amesema hadi jana hatua iliyokuwa ikiendelea chini ya uratibu wake, ilikuwa ni Shirika hilo la Madaktari wa Stemm kutoka Marekani kupata hospitali itakayowapokea watoto hao.
