Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, leo amewaapisha Mawaziri 21 na Manaibu Waziri 21 aliowateua, baada ya kufanya mabadiliko ya Baraza hilo Oktoba 7 mwaka huu.
Sherehe za kuapishwa kwao zimefanyika Ikulu jijini Dar es salaam,na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa, wakiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma.
Miongoni mwa viongozi waliopata kuzungumza katika hafla hiyo ni Spika wa Bunge la Jamhuri la Tanzania Mh Job Ndugai, na yeye amewataka kuchapa kazi ili kuleta maendeleo kwa Taifa, na kumpongeza katibu wa Bunge aliyemaliza muda wake Mh Thomas Kashilila na kumkaribisha Katibu mpya wa Bunge Mh Gaigai.
Kiongozi mwingine aliyepewa nafasi na Rais Magufuli kuzungumza ni Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Juma, ambaye amewapongeza na kuwatikia kuwajibika katika kazi, na kuwataka kufuata sheria, katiba na taratibu ili kuondoa migongano na mahakama.
