JUMLA ya vituo 710 vya mafuta vilifungwa nchi nzima tangu ianze kazi ya kuvikagua vituo hivyo kuona kama vinatumia mashine za kieletroniki za malipo (EFDs).
Vituo 469 kati ya hivyo vimefunguliwa baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na Mamlala ya Mapato Tanzania (TRA), ambavyo ni kulipia gharama za ufungaji mashine hizo kwa mawakala walioidhinishwa na TRA kisha kuingia makubaliano ya muda maalumu wa kuhakikisha kuwa mashine hizo zimefungwa.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya, makubaliano hayo ya muda maalumu yanamruhusu mmiliki wa kituo cha mafuta kuendelea kutumia mashine za kawaida mpaka hapo mashine za kisasa zitakapofungwa.
Aidha, Kamishna Mwandumbya amesema wamiliki wa vituo vya mafuta ambao watashindwa kutekeleza agizo la kufunga mashine za malipo za kielektroniki za kutolea risiti kwa muda uliowekwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa vitu vyao na kufikishwa mahakamani.
Aidha amesema muda waliopewa kufunga mashine hizo hautaongezwa na wamiliki wanapaswa kulizingatia hilo ili kuepuka adhabu, na kwamba baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo wamekuwa siyo waaminifu kwa kuzificha mashine hizo ndani badala ya kuzifunga kwenye pampu na wengine wamezifunga, lakini hawakuziunganisha na pampu.
Mwandumbya alisema asilimia 70 ya vituo vya mafuta nchini vinamilikiwa na kuendeshwa na wajasiriamali wadogo wanaojulikana kama DODO (Dealer Owned Dealer Operated).
